Gesi Asilia

Gesi Asilia | Udhibiti wa Kiufundi | Utoaji wa Leseni za Gesi Asilia | Nyenzo za Udhibiti | Udhibiti Uchumi | Utatuzi wa Malalamiko na Migogoro

Taarifa za Jumla

Mamlaka ina jukumu la kudhibiti shughuli za mkondo wa kati na wa chini za gesi asilia zinazojumuisha usindikaji, usafirishaji, uhifadhi na usambazaji wa gesi asilia nchini. Miundombinu inayodhibitiwa ni pamoja na mitambo ya usindikaji, bomba la usafirishaji, usambazaji na vifaa vya kuhifadhi.

Tanzania imekuwa ikifanya utafiti wa gesi asilia kwa zaidi ya miaka 50. Ugunduzi wa kwanza wa gesi asilia nchini ulifanyika mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songo Songo kilichopo Mkoa wa Lindi na kufuatiwa na ugunduzi wa pili katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara mwaka 1982. Gesi asilia kutoka Songo Songo iliuzwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na ya kutoka Mnazi Bay mwaka 2006. Ugunduzi huo umechochea kufanyika utafiti zaidi wa gesi asilia kwa maeneo ya nchi kavu na majini.

Wapo watoa huduma wanne wanaotekeleza shughuli za gesi asilia  katika mkondo wa kati na wa chini. Watoa huduma hao ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Songas Limited, Pan African Energy Tanzania Limited (PAET), na Maurel & Prom (M&P). Zipo kampuni zinazoendelea kufanya utafiti baharini na nchi kavu ni Ophir Energy plc, Shell/BG Group plc (BG), Statoil, ExxonMobil, na Ndovu Resources (Aminex).

Hadi kufikia Machi 2016, Wizara ya Nishati ilithibitisha kuwa, hifadhi ya gesi asilia iliyogunduliwa inafikia futi za ujazo trilioni 57.25.

Visits: 1190