Rejesta ya Watoa Huduma katika Miradi ya Mafuta na Gesi Asilia Nchini

Rejesta ya Watoa Huduma katika Miradi ya Mafuta na Gesi Asilia Nchini

 

Usajli wa wagavi na watoa Huduma katika miradi ya mafuta na gesi asilia nchini (LSSP), ni mchakato unaofanywa na Mamlaka kusajili wasambazaji na watoa huduma wote wa ndani, wenye sifa zinazostahili kuingizwa kwenye hazinadata iliyotengenezwa na Mamlaka, ili waweze kutoa huduma inayohitajika katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini. LSSP pia, ni sharti ambalo limebainishwa na Sheria ya Petroli, (the Petroleum Act, 2015) katika utekelezaji wa falsafa ya kushirikisha watoa huduma wa ndani.

Ushirikishwaji wa watoa huduma wa ndani inajumuisha kuendeleza ujuzi, ubadilishanaji wa teknolojia ya mafuta na gesi asilia, na matumizi ya wataalamu wa ndani katika uzalishaji.

Sheria ya Petroli, (the Petroleum Act, 2015) inaeleza namna Serikali inavyoweza kushiriki katika shughuli za petroli. Vifungu vya 218 hadi 224 cha Sheria ya Petroli, (the Petroleum Act, 2015) vinafafanua dhana ya ushirikishwaji, wajibu wa kukuza maslahi ya nchi, chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA); Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Pia, inaweka wajibu kwa wenye leseni kuandaa na kuwasilisha mpango wa ushirikishaji wazawa kwa PURA au EWURA.

Kwa ufafanuzi zaidi, inaweza kuelezwa kwamba, ushirikishwaji wa watoa huduma wa ndani ni falsafa ya kujenga nguvu kazi iliyo na ujuzi na msingi wa ushindani wa wasambazaji na watoa huduma. Hili limekuwa suala muhimu sana kutokana na ukweli kwamba, katika zama hizi, kila nchi ingependa raia wake kushiriki katika viwango vya juu vya uchumi wake na hivyo kusaidia kubaki na utajiri wake ndani ya mipaka yake, pamoja na kutoa ajira kwa kuzingatia ongezeko la idadi ya watu

 

Kanuni za Petroli (the Petroleum Local Content Regulations, 2017) zinaeleza namna taarifa katika tasnia ya petroli zinaweza kupatikana kupitia mfumo wa pamoja wa taarifa uitwao Common Qualification System (CQS).

Hata hivyo, mchakato huu, haukusudii kuchukua nafasi ya Common Qualification System (CQS).

Kwa mujibu wa Kanuni ya 38 ya Kanuni za Petroli (the Petroleum Local Content Regulations 2017) EWURA ina jukumu la kutunza hazinadata yenye maelezo ya wazabuni wa ndani, watoa huduma na taasisi nyingine zinazokidhi matakwa ya kutoa huduma katika tasnia ya petroli na gesi asilia nchini.

Hazinadata ya LSSP ni nyenzo ya udhibiti inayoisaidia EWURA kusimamia uzingatiaji wa masharti ya leseni na mikataba ya watoa huduma ili kuweka kipaumbele katika matumizi ya bidhaa za ndani, kazi na huduma kwa kuzingatia masharti yaliyoanishwa na Kanuni za Petroli (the Petroleum Local Content Regulations, 2017) (GN-197).

Uhakiki wa awali ni sehemu ya mchakato wa zabuni unaobainisha iwapo kampuni ina sifa zinazotakiwa kutoa huduma. Hazinadata itakuwa chombo pekee cha rejea ya sifa ya kutoa huduma katika tasnia ya mafuta na gesi asilia nchini

Hivyo, ni kosa kwa kampuni zisizosajiliwa katika hazinadata ya EWURA kutoa huduma katika miradi ya sekta ndogo za petroli na gesi asilia nchini.

 

Hits: 478