Maelezo ya Jumla

Maelezo ya Jumla

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ni taasisi ya udhibiti wa huduma za nishati na maji inayojitegemea, iliyoundwa kwa Sheria ya EWURA Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania na marekebisho yake Na. 6 ya mwaka 2019.

EWURA, ilianza kazi rasmi Septemba, 2006 ikiwa na wajibu wa kusimamia shughuli zote za kiuchumi na kiufundi katika sekta za Nishati(umeme, petroli na gesi asilia); na Maji (majisafi na usafi wa mazingira).

Katika kutekeleza wajibu wake, kwa uwazi na kwa manufaa ya wote, EWURA inazingatia sheria za kisekta, sera na miongozo ifuatayo:-

Sera ya Taifa ya Nishati (2015), Sera ya Taifa ya Maji (2002), Sheria ya EWURA, Sura Na. 414; Sheria ya Umeme, Sura Na. 131; Sheria ya Petroli, Sura Na. 392; Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira, Sura Na. 279;  kanuni na miongozo  mbalimbali.

Dira ya EWURA

Kuwa Mdhibiti wa Kiwango cha Kimataifa kwa Huduma Endelevu za Nishati na Maji

Dhamira ya EWURA

Kudhibiti huduma za nishati na maji kwa uwazi, ufanisi na tija ili kuhakikisha ubora, upatikanaji na unafuu wa huduma hizo

 

Kazi na Majukumu ya EWURA

Kwa mujibu wa Kifungu cha 7 cha Sheria ya EWURA, majukumu ya Mamlaka niajukumu hayo ni:-

  • Kutekeleza kazi zote zilizoanishwa kwenye sheria ya EWURA na Sheria za Kisekta;
  • Kutoa, kuhuisha na kufuta leseni;
  • Kuweka na kusimamia viwango vya ubora wa huduma;
  • Kudurusu na kusimamia bei za huduma,
  • Kutunga sheria ndogo na kanuni;
  • Kufuatilia maendeleo ya sekta zinazodhibitiwa kwa kuzingatia upatikanaji, ubora wa huduma, gharama ya huduma, ufanisi wa uzalishaji, uwekezaji na usambazaji wa huduma;
  • Kusimamia utatuzi wa malalamiko na migogoro;
  • Kutoa taarifa kuhusu kazi za udhibiti;
  • Kupata maoni ya mamlaka zingine za kiudhibiti; na
  • Kusimamia utekelezaji wa Sura Na 414 ilyoianzisha EWURA.

 

Katika kutekeleza kazi zake, EWURA ina wajibu wa kukuza ustawi wa Watanzania kwa kuzingatia yafuatayo:-

  • Kuhimiza ushindani wenye tija na ufanisi kiuchumi;
  • Kulinda maslahi ya walaji;
  • Kulinda mitaji ya kifedha ya watoa huduma;
  • Kuhimiza upatikanaji wa huduma zinazodhibitiwa kwa makundi yote ikiwamo wenye vipato vya chini,makundi maalumu na vijijini;
  • Kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma na kujenga uelewa kuhusu sekta zinazodhibitiwa, ikiwamo haki na wajibu wa watumiaji na watoa huduma zinazodhibitiwa, namna ya kupokea na kutatua malalamiko na migogoro na kazi, wajibu na shughuli za Mamlaka;
  • Kulinda na kutunza mazingira.

 

Hits: 30225