Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji

"Udhibiti wa Haki kwa Matokeo CHANYA"
Miundombinu ya petroli

Miundombinu inayohusika na bidhaa za petroli ni pamoja na gati la kupokelea mafuta, maghala ya kuhifadhi, vyombo vya usafirishaji, vituo vya mafuta vya rejareja na vya matumizi binafsi.

Miundombinu ya kupokelea bidhaa za petroli

Miundombinu inayotumika kupokelea meli zinazoleta bidhaa za petroli ipo katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Bandari ya Mtwara ilianza kupokea bidhaa za petroli Julai 2018 na kuwa bandari ya tatu kwa Tanzania Bara baada ya bandari ya Dar es Salaam na Tanga. Bandari ya Mtwara inahudumia mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Bandari ya Tanga inahudumia Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara wakati Bandari ya Dar es Salaam inahudumia mikoa mingineyo pamoja na nchi jirani. Bofya hapa kuona kiwango cha juu cha uwezo wa kufanya kazi kwa usalama na bidhaa zinazopokewa kwenye gati ya kila bandari.

Ghala za kuhifadhi bidhaa za petroli

Tanzania Bara ina maghala 23 za kupokelea mafuta zilizopo katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, zenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo  1,637,222. Ghala hizi hupokea bidhaa za petroli kutoka melini. Aidha, kuna ghala 29 nchi kavu, zenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 75,625. Hata hivyo, ghala hizo, nyingi hazifanyi kazi. Pia, Kampuni ya Bomba la Mafuta la TAZAMA inapokea mafuta ghafi kupitia boya (SBM) na kuhifadhi bidhaa hizo kwenye ghala lake lenye mita za ujazo 231,000.

Miundombinu ya usafirishaji bidhaa za petroli

Duniani kote  zipo njia kuu nne za usafirishaji wa bidhaa za petroli ambazo ni bomba, reli, barabara na maji. Licha ya kuwepo njia mbalimbali za usafirishaji kwa sasa, , barabara inategemewa zaidi kuwa ndiyo njia kuu ya kusafirisha bidhaa za petroli Tanzania Bara. Malori hutumika kusafirishia bidhaa za petroli kutoka kwenye maghala ya kupokelea (Dar es Salaam, Tanga na Mtwara) kwenda kwa watumiaji nchini kote na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, DR Congo na Uganda.

Aidha, lipo bomba la TAZAMA linalosafirisha mafuta ghafi kutoka Kigamboni, Dar es Salaam hadi Ndola, Zambia.

Vituo vya mafuta

Vituo vya mafuta, ni sehemu ya mwisho kabla ya bidhaa za petroli kumfikia mteja. Hadi tarehe 30Septemba, 2024, kulikuwa na vituo 2,405 vyenye leseni ya kuuza mafuta rejareja  Tanzania Bara. Mwenendo unaonyesha kuwa uwekezaji katika vituo vya mafuta nchini kote unakua, kutokana na ongezeko la mahitaji ya mafuta

Vituo vya gesi ya kupikia inayotokana na  petroli (LPG)

Uwekezaji katika gesi ya kupikia (LPG) itokanayo na mafuta ghafi  unalenga kuhakikisha kuwa, gesi hiyo ambayo ni safi, inayozingatia kanuni za afya, usalama, mazingira. Pia, inapatikana kwa urahisi kwa watumiaji wa nyumbani na gharama nafuu ikilinganishwa na matumizi ya kuni, mkaa na mafuta ya taa.

Hadi kufikia 31 Desemba 2024, kulikuwa na maghala (6) za kuhifadhi gesi ya kupikia yaliyopo. Dar es Salaam na Tanga yenye uwezo wa kuhifadhi tani za ujazo 17,770. Pia, vipo vituo 37 vya kuhifadhi na kujazia gesi nchini, vyenye uwezo wa jumla ya tani za ujazo 2214.