Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji

"Udhibiti wa Haki kwa Matokeo CHANYA"
Nyenzo za Udhibiti

Uanzishwaji na majukumu ya EWURA ni kwa mujibu wa sera na mifumo ya kisheria. Vyombo vya udhibiti vinavyoongoza na kusaidia Mamlaka kutekeleza kwa ufanisi na tija majukumu yake ya udhibiti katika mkondo wa kati na chini wa sekta ndogo ya mafuta ni pamoja na Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015, sheria za sekta na viwango vilivyoandaliwa. Maelezo zaidi yako hapa chini.

Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015

Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 ilitokana na muunganiko wa sera mbalimbali za sekta ndogo za nishati ambazo ni: Sera ya Mafuta, Sera ya Ushiriki wa Watanzania, Sera ya Gesi Asilia, Sera ya Nishati Mbadala, na Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2003. Lengo kuu la kuunganisha sera hizi za sekta ndogo za nishati lilikuwa ni kurahisisha usimamizi wake na kuboresha utawala na utendaji wa sekta hiyo.

Sera inatoa mwelekeo sahihi kwa maendeleo ya sekta ya nishati kwa ujumla kwa lengo kuu la kuanzisha uzalishaji bora wa nishati, ununuzi, usafirishaji na usambazaji wa nishati kwa kuzingatia njia rafiki kwa mazingira. Kupitia Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015, mfumo wa kisheria na wa udhibiti pamoja na taasisi za kusimamia mkondo wa kati na chini wa sekta ndogo ya mafuta uliwekwa wazi.

Sheria na Kanuni

Mfumo wa kisheria kwa ajili ya mkondo wa kati na chini wa sekta ndogo ya mafuta umegawanyika katika makundi mawili: sheria mama na sheria ndogo. Sheria mama ni zile zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku sheria ndogo zikiwa ni Kanuni zilizotungwa na Waziri mwenye dhamana ya mafuta na Kanuni za Ndani zilizotungwa na Mamlaka.